Darpori kijiji chenye watu 10,000 ambacho hakina huduma ya afya tangu uhuru

Standard

Picha inakionesha kijiji cha Darpori kilichopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma,kijiji hiki kina watu 10,000 kipo mpakani mwa nchi za Tanzania na Msumbiji,tangu uhuru hadi sasa kijiji hiki licha ya kuwa na utajiri wa milima yenye dhahabu na idadi kubwa ya watu hakina huduma yeyote ya afya hali ambayo inaathiri ustawi wa jamii ikiwa ni pamoja na watu kupoteza maisha. 

-Wajawazito wanasafiri kilometa 18 kufuata huduma ya uzazi

Na Albano Midelo

WAHENGA walisema tembea uone mambo,ndivyo nilivyofanya mimi kufunga safari kutoka mjini Songea hadi kufika katika kijiji cha Darpori wilayani Mbinga mkoani Ruvuma umbali wa  takribani kilometa 200.

Kijiji cha Darpori kipo mpakani mwa Tanzania na nchi ya Msumbiji ,kutoka katika kijiji hicho kueleka nchini Msumbiji kwa mguu ni dakika 60,wakazi wa kijiji hiki ni wageni ambao wamefika katika kijiji hicho kwa ajili ya kufanyakazi ya uchimbaji na ununuzi wa madini mbalimbali yakiwemo  dhahabu ambayo yanapatikana kwa wingi katika kijiji hicho.

Mwenyekiti wa kijiji cha Darpori Andason Haule anasema kijiji hicho chenye watu karibu 10,000 kilianza rasmi mwaka 2004 kikitokana na eneo ambalo ulikuwa msitu kugundulika kuwa na mkondo wa madini mengi aina ya dhahabu na kwamba kijiji kina karibu makabila yote 120 yaliopo nchini pamoja na wananchi kutoka nchi jirani za Malawi na Msumbiji.

Kijiji cha Darpori kilichopo katika kata ya Tingi wilayani Mbinga mkoani Ruvuma kinachoundwa na vitongoji vinne ambavyo ni Songeapori,Lunyere,Tanzania One na Njarambe,katika hali ya kusikitisha hakina kituo chochote cha kutolea huduma ya afya hali ambayo inasababisha matatizo mengi kwa wakazi wa kijiji hicho ikiwemo kusababisha vifo ambavyo vingeweza kuzuilika.

Mwenyekiti wa kijiji hicho anasema akinamama wajawazito wanasafiri umbali wa kilometa  18 hadi kijiji  jirani cha Mpepo ambako kuna zahanati ya kanisa katoliki kwa ajili ya kwenda kupima kliniki watoto pamoja na kupata huduma ya uzazi na kwamba katika kijiji hicho kuna mkunga wa jadi ambaye wakati mwingine anawasaidia akinamama kujifungua hata hivyo wengi wanapoteza maisha kila mwaka.

“Hapa kijijini makaburi ya akinamama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano imekuwa ni jambo la kawaida ,sisi viongozi tupo katika wakati mgumu tunashindwa hata kuitisha mikutano ya hadhara kwa kuwa kwenye mikutano hiyo kilio kikubwa cha wananchi ni kupata zahanati  hivi sasa wanatumia shilingi 20,000 nauli ya kwenda na kurudi hadi kwenye zahanati ya Mpepo kufuata huduma ya afya hali ni mbaya’’,anasisitiza.

“ wanawake wamekuwa wakitoa kilio chao kwamba  serikali ya kijiji haifanyi kazi wanakufa njiani kutokana na kijiji hicho kukosa zahanati sasa mimi mwenyekiti wa kijiji nitafanya nini ,mbunge ameshaambiwa mara kadhaa,viongozi ngazi ya wilaya wameambiwa lakini ahadi zimekuwa nyingi kuliko utekelezaji’’,anasema.

Joyce Nchimbi mama mwenye watoto wanne  anasema hali ya afya ni mbaya zaidi wakati wa mvua kwa kuwa barabara inakuwa haipitiki hivyo akinamama wengi wanashindwa kusafiri kutoka katika kijiji hicho hadi Mpepo kwenda kujifungua au kupima kliniki wao wenyewe pamoja na watoto wenye umri chini ya miaka mitano hali ambayo inaleta hofu katika hustawi wa jamii.

Hata hivyo afisa mtendaji wa kijiji cha Darpori  Raphael Mapunda anasema katika kukabiliana na  tatizo la huduma ya afya serikali ya kijiji imehamasisha wananchi katika vitongoji vyote vinne  kufyatua tofali 700,000 za ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Tingi na hatimaye kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo la ukosefu wa  huduma ya afya ambalo linatafuna maisha ya watu mara kwa mara.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Tingi Aureus Masuja anasema kata hiyo yenye vijiji nane ambavyo ni Darpori, Tingi, Kiulunga, Mpepo, Malungu, Upolo, Kilindinda na Luhindo tangu nchi ipate uhuru haijawahi kupata zahanati ya serikali badala yake katika kata nzima yenye watu zaidi ya 16,000 inategemea zahanati mbili za kanisa katoliki ambazo zipo kwenye vijiji vya Mpepo na Tingi.

“Tangu tupate uhuru hatujawahi kuwa na hospitali au zahanati ya serikali ,katika huduma ya afya katika kata nzima tunasaidiwa na zahanati mbili za kanisa katoliki,hatujawahi kuwa na mradi wa zahanati,hata hivyo miradi ya zahanati imeanza katika vijiji vya  Upolo na Kilindinda zahanati zimefikia hatua ya ujenzi wa msingi,mradi wa zahanati  katika kijiji cha Luhindo wamefikia hatua ya madirisha pia mradi wa kituo cha afya cha kata katika kijiji cha Darpori ufyatuaji wa tofali unaendelea’’,anasisitiza.

Masaju anabainisha kuwa huduma za afya zinazotolewa katika zahanati mbili za kanisa katoliki  kwa wananchi wa kata nzima  bado hazikidhi ukubwa wa eneo la kata nzima ya Tingi hali ambayo inawalazimisha wananchi kufunga safari ya kwenda mjini Mbinga kufuata matibabu ya uhakika na kwamba wananchi wanapata athari kubwa ambapo wajawazito wengi wamekuwa wanajifungulia barabarani au kupoteza maisha wakati wanakwenda kutafuta huduma za afya.

Anasisitiza kuwa  idadi kubwa ya watoto wachanga wanateketea kwa kupoteza maisha kutoka na ugonjwa wa malaria ambao unaongoza kwa kuwashambulia wananchi wa kata hiyo ukilinganisha na magonjwa mengine.

Ametoa mwito kwa serikali ya Halimashauri ya wilaya ya Mbinga kuhakikisha kuwa wanawaunga mkono wananchi wa kata ya Tingi ili kuhakikisha kuwa  miradi yao ya ujenzi wa zahanati pamoja na kituo cha afya inamalizika kwa muda uliopangwa ili hatimaye huduma za afya zianze kutolewa jirani na wananchi na kupunguza au kumaliza vifo visivyokuwa vya  lazima ambavyo vinamaliza nguvu kazi ya taifa kila mwaka.

Mwandishi anapatikana kwa simu 0766463129 barua pepe albano.midelo@gmai.com

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s